Fahamu tahadhari aliyoitoa Nyerere kuhusu mgogoro wa mashariki ya DRC

Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda sasa wanaudhibiti na kuuendesha mji wa Goma ambao ndio mkubwa na muhimu zaidi katika eneo la mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Mji wa Goma ndio makao makuu ya kiutawala wa jimbo la Kivu Kaskazini na baada ya Kinshasa na Lubumbashi, Goma ni mji wa tatu kwa ukubwa nchini DRC. Pia ni kitovu cha biashara kubwa ya madini ikiwa ni pamoja na dhahabu, coltan, bati na biashara za madini mengine kutoka migodi tajiri huko Masisi, Walikale na kwingineko katika mkoa huo.
Ni makao ya mashirika mengi ya kimataifa ya misaada na ni kituo cha jeshi la Umoja wa Mataifa jeshi kubwa zaidi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani (MONUSCO) Pamoja na vikosi vya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Africa (SADC) kutoka Afrika Kusini, Tanzania, na Malawi vipo katika mji huo.
Hivyo, kuanguka kwa Goma ni dhahiri kuwa ni pigo kubwa kwa serikali ya Kinshasa pamoja na washirika wake. Lakini pia hatua muhimu ya kusukuma ajenda ya kundi la M23 pamoja na washirika wake katika mgogoro wao na serikali ya nchi hiyo.Swali muhimu zaidi ni kuwa wakati vita ikiendelea – japo M23 wametangaza kusitisha mapigano wakati wakiwa njiani kujaribu kuuteka mji mwingine muhimu wa Bukavu uliopo katika jimbo la Kivu Kusini – je, M23 kuiteka Goma pamoja na miji na vijiji vingine katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini kunaweza kuleta suluhu ya vita?
Je, kutekwa kwa mji wa Goma mara hii kutaleta mabadiliko yoyote?

Kujibu swali hili ni muhimu kuangalia kiini cha mzozo wenyewe kwani hii ni mara ya pili kwa M23 kuuteka mji wa Goma. Mnamo mwezi wa Novemba, 2012, M23 iliuteka mji huu kwa siku 10, baada ya majeshi ya DRC kuutoroka, lakini baadaye waliondoshwa na kikosi maalumu cha kulinda amani cha kikanda kilichokuwa chini ya mwamvuli wa MONUSCO ambacho kilijumuisha wanajeshi wa Tanzania, Afrika Kusini na Malawi.
Hali inavyoonesha ni kuwa mwaka huu – tofauti na ilivyokuwa mwaka 2012 – M23 hawana mpango wa kuishikilia Goma kwa muda mfupi –kwa kuwa tayari wamesogeza mstari wa mbele wa mapambano kuelekea Bukavu. Japo katika tangazo lao la kusitisha mapigano la Jumatatu usiku wametangaza kuwa hawana nia ya kuuteka mji wa Bukavu.
Lakini katika tangazo hilo hilo, wamelaani kile walichodai ni jeshi la Kongo kutuma ndege za kivita "kuua watu katika maeneo ambayo yamekombolewa." Kwa mujibu wa M23, ndege hizo zinatokea katika kiwanja cha ndege cha Kavumu ambacho kipo karibu na Bukavu.
M23 pia wameendelea kusisitiza pia kuwa SADC inapaswa kuondoa vikosi vyake (kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi) wakisema misheni yao DRC haina uhalali tena.
SADC pamoja na jumuiya nyingine za kikanda na kimataifa zikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), nchi zenye Uchumi mkubwa zaidi duniani (G7) na UN wamelaani vita vinavyoendelea na kutaka mapigano yasitishwe. Wote wanalaani waasi kuteka maeneo ya nchi yaliyo chini ya serikali halali ya DRC.
Rwanda, imekuwa ikisisitiza kuwa kinachoendelea DRC ni tatizo la ndani ya DRC na linatakiwa lisuluhishwe na serikali ya nchi hiyo
ambayo wanadai imeshindwa kufanya hivyo na kuwalazimu M23 kudai haki zao kwa mtutu wa bunduki.
Jumuiya ya kimataifa pia ilipinga vikali mwaka 2012 M23 kuteka maeneo yan chi hiyo ikiwemo Goma na hatua kadhaa kuchukuliwa ikiwemo kushambuliwa kwa M23 japo suluhisho la kisiasa halikupatikana.
Swali gumu katika mgogoro unaondelea sasa ni je, suluhu ya kudumu ya kisiasa itapatikana?
'Kiini ni mauaji ya kimbari na ubaguzi'

M23 inasema kuwa inapigania maslahi ya Wakongomani wanaozungumza Kinyarwanda, wakisema kuwa wanaonyanyaswa na hata kuuliwa na serikali ya Kinshasa.
Waasi wa M23 pia wanailamu serikali ya DRC pia kuyaunga mkono makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao nchini Kongo, wakiwemo wapiganaji wa jamii ya Kihutu kutoka Rwanda waliotorokea DRC mwaka 1994 baada mauaji ya kimbari, kuwaangamiza ili kuwalazimisha kurudi Rwanda, shutuhuma ambazo serikali ya DRC inazikanusha.
Madai hayo mawili pia yanaungwa mkono na Rwanda, na ndiyo chimbuko la nchi hiyo kuhusishwa na kulaumiwa kwa kuwaunga mkono na kuwafadhili waasi wa M23 na harakati zao nchini DRC.
Rwanda inailaumu DRC kuwakumbatia na hata kuwaingiza katika jeshi lake la wanamgambo wa Kihutu chini ya kikundi cha FDLR hali inayohatarisha usalama wake. DRC inakanusha shutuma hizi.
Uhusiano wa karibu wa Rwanda na M23 unathibitika pia kwa ukaribu wa baadhi ya wakuu kundi hilo na utawala wa Kigali. Kamanda mkuuwa kijeshi wa M23 Sultani Makenga, alipigana chini ya Paul Kagame wakati huo akiongoza waasi kutwaa madaraka Kigali dhidi ya iliyokuwa serikali ya Rwanda na kukomesha mauaji ya Kimbari mwaka 1994. Na baada ya hapo, Makenga pamoja na Banyamulenge wengine waliomuunga mkono Kagame walijiunga na makundi mengine ya wanamgambo na kushirikiana na jeshi la Rwanda kumpindua Mobutu Sese Seko na hatimaye kumuwezesha Laurent-Désiré Kabila kuingia madarakani.
Suala la ubaguzi dhidi ya Wakongomani wanaozungumza Kinyarwanda (Wanyamulenge) lipo tangu enzi ya utawala wa Mobutu Sese Seko, DRC ikiitwa Zaïre. Wanyamulenge wanaozungumza Kinyarwanda wanaopatikana zaidi katika maeneo ya Kivu wamekuwa wakisema wamenyanyaswa tangu miaka ya 1960 na wamekuwa wakiambiwa "warudi nyumbani" Rwanda.

Wanyamulenge walijipata upande wa Congo wakati wakoloni walipokata mipaka mipya ya mataifa ya Afrika katika miaka ya 1900. Baadhi ya wenyeji wa ufalme wa zamani wa Rwanda kutoka kabila la Abanyamulenge ndio wanaounda kundi la M23.
Akielezea chanzo cha tatizo la Wanyamulenge katika mkutano ulioandaliwa New York na taasisi ya amani, International Peace Academy mwaka 1996, aliyekuwa Rais wa Tanzania Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliilaumu serikali ya Zaïre kwa kusababisha mzozo wa ya kikabila kwa kushindwa kusitisha unyanyasaji.
''Wanyamulenga sio wahamiaji waliokuja Zaïre. Ufalme wa Rwanda uliganywa kati ya Ubelgiji na Ujerumani. Na Ubelgiji ulichukua theluthi mbili ya ufalme wa Rwanda…Tunaposema heshimu mpaka uliowekwa na Ujerumani na Ubelgiji, pia tunapaswa kuwaheshimu watu uliowapokea chini ya mgawanyo'', alisema Nyerere na kuongeza kuwa: Huwezi kugeuka na kusema si raia wa nchi hii. Je utawarejesha peke yao au utawarudisha na kipande chao cha ardhi?...huwezi kusema nenda nyumbani!, nyumbani wapi?''.
Katika kujenga hoja yake, Nyerere alitoa mfano wa kabila la Wamasai wa Tanzania na Wamasai wa Kenya na kusema hawawezi kuambiwa warudi Kenya ama Tanzania kwa kuwa nchi yao ya asili iligawanywa katika makoloni mawili ya Waingereza na Wajerumani na baada ya uhuru wamejikuta wapo katika nchi mbili tofauti.
Je, suluhu ya mzozo huu inaweza kupatikana?

Juhudi za upatanishi wa kikanda juu ya utatuzi wa mzozo wa DRC, M23 na Rwanda kupitia mazungumzo ya Nairobi na ya Luanda yaliyoongozwa na Rais wa Angola João Lourenço na Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta na kutumwa kwa vikosi vya Afrika Mashariki, na vile vya SADC zimeshindwa kupata suluhu ya amani kufikia sasa katika eneo hilo la mashariki mwa DRC.
Kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kinachofahamika kama MONUSCO ambacho kimekuwa DRC kwa miaka takriban 30 pia kimeshindwa kumaliza mzozo wa Mashariki mwa DRC.
Pande zote pia zimekuwa zikilaumiana kwa kukiuka makubaliano ya amani, ambayo yangeweza kuleta suluhu la mzozo huo.
Mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia Dkt. Nicodemus Minde anasema suluhu la mzozo wa DRC litapatikana kwa njia ya kisiasa na kidiplomasia na sio kwa hatua za kijeshi ambazo zimekuwa zikishuhudiwa.
Jambo la kwanza ''Kunapaswa kuwa na muktadha wa kufahamu ni nini kinachoendelea, Rwanda, DRC – Kwa wasuluhishaji ni muhimu kuangalia chimbuko kihistoria zaidi na kufahamu chimbuko la mzozo. Tukifahamu historia ya vita na malumbano itakuwa ni njia nzuri'', anasema Dkt. Minde.
Kulingana naye suluhu ya sasa ni kuwakutanisha mahasimu na kuwaleta katika meza ya mazungumzo. Hata hivyo anasema mzozo huu hauna suluhisho moja tu.
''Mzozo huu unahitaji suluhisho la usitishaji mapigano, suluhisho la muda mfupi la utekelezaji wa michakato ya amani inayoendelea kwa mfano mchakato wa Luanda uliokwama kutokana na Rwanda kutokubaliana nao, na mchakato wa Nairobi uliosusiwa na Rais wa DRC Felix Tschidekedi''.
Aidha anasema suluhu nyingine inayoweza kudumu ni ''Kuiunganisha michakato hii miwili ambayo itawaleta wahusika wa mzozo huu kutoka EAC na SADC kwa kuwa ndio wanaoelewa zaidi hali halisi ya mzozo wa DRC na chimbuko lake.''
Viongozi wa SADC na EAC wanatarajiwa kukutana jijini Dar Es Salaam Ijumaa na Jumamosi ya wiki hii kujadiliana kuhusu mgogoro huo.
Funzo lililopatikana miaka 12 iliyopita ni kuwa vita peke yake haviwezi kumaliza mgogoro huu.
Maoni